Dar es Salaam.Wakati Yanga ikiikabili JKT Tanzania ugenini kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaofanyika Uwanja wa Mkwakwani Tanga, timu hiyo ina asilimia kubwa ya kushinda mchezo wa leo.

Kwa miaka saba, JKT Tanzania (zamani Ruvu JKT) haijawahi kushinda dhidi ya Yanga kwenye Ligi Kuu Bara na zinapokutana leo Yanga inaonekana itaingia kwa hasira kubwa ili kupata ushindi na kupoza machungu baada ya michezo mitatu iliyopita kufanya vibaya.

Yanga ilipoteza dhidi ya Stand United kwa bao 1-0, kisha ikatoka sare ya bao 1-1 na Coastal Union na kutoka suluhu na Singida United hivyo hivi sasa ina pointi 55 ikiizidi Simba pointi 19.

Mara ya mwisho JKT Tanzania kuifunga Yanga kwenye Ligi Kuu ilikuwa Agosti 21 mwaka 2011 iliposhinda bao 1-0.

Baada ya hapo ni vipigo tu vikawa vinatembea na kuanzia mwaka 2012 mpaka leo, Yanga imeifunga JKT Tanzania mabao 42 wakati wanajeshi hao wakiwafunga wapinzani wao mabao sita tu.

Jambo hilo linawafanya Yanga kuingia katika mchezo wa leo ikijiamini ingawa kwenye soka lolote linaweza kutokea narekodi huwekwa ili zivunjwe.

Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera ni kama ametangaza hali ya hatari kwa JKT Tannzania baada ya kusema matokeo mabaya mfululizo waliyoyapata hayawakatishi tamaa bali yamewapa nguvu ya kuingia katika mchezo wa huo na kushinda.

Zahera anaamini matokeo hayo yatakuwa somo kwa wachezaji wake na kuongeza juhudu ya kupambana uwanjani ili kuondoka na pointi tatu leo na kurejesha furaha kwa mashabiki wao.

“Yaliyopita yamepita sasa tunaangalia mechi zinazokuja tukianza nah ii ya JKT Tanzania. Itakuwa mechi ngumu kwani ni timu nzuri na kila wakati lazima umuheshimu mpinzani wako.

“Tunachotakiwa ni kuhakikisha tunashinda mchezo huo. Morali ya wachezaji wangu iko juu na naamini watapambana uwanjani na kuweza kushinda mchezo huo.

Zahera leo atamkosa mshambuliaji wake Mcongo Heritier Makambo mwenye kadi tatu za njano na kiungo Thaban Kamusoko mwenye maumivu ya nyama za paja.

Pia Zahera anaweza kumtumia kiungo, Mohammed Issa ‘Banka’ ambaye hivi sasa yuko huru baada ya kumaliza adhabu yake ya kufungiwa mwaka mmoja kwa kosa la kutumia madawa yasiyotakiwa michezoni na tayari Shirikisho la Soka Tanzania(TFF) limewatumia Yanga leseni ikiwa na maana kuwa anaweza kuanza kuitumikia timu hiyo.

Kocha wa JKT Tanzania, Bakari shime alisema anaiheshimu Yanga lakini hawatakubali kufungwa kwani wanataka kuendeleza rekodi yao nzuri ya michezo minne iliyopita.

Katika michezo minne iliyopita ya hivi karibuni, JKT Tanzania imeshinda michezo mitatu na kutoa sare mchezo mmoja.Source link