Aisha Bakari Mohamed maarufu kama DJ baby mama ni msichana wa kwanza wa kizanzibari anaefanya shughuli za kupiga muziki katika maeneo mbalimbali (DJ).

Huvalia mavazi ya kujistiri ikiwemo hijab wakati wa kazi zake, na kupiga muziki katika maeneo ya starehe kama vilabu na migahawa.

Hijab ni vazi la wanawake wa Kiislam ambalo hutumia kujifunika maeneo ya mwili ama kujistiri, Aisha hutumia vazi hilo hata akiwa katika kazi zake, ikiwemo kupiga muziki kwenye vilabu vya burudani.

Aisha anaipenda sana kazi hii, mbali na kuwa haiendani na utamaduni wa visiwa vya Zanzibar ambapo idadi kubwa ni jamii ya Kiislam.

Baadhi ya ndugu na watu wa karibu wamekua wakimshauri kuachana na kazi hii, kwani haiendani na maadili ya kizanzibari.

Aisha Bakari Mohamed
”Ni jambo la ajabu, unavaa baibui halafu unapiga muziki kwenye vilabu”anasema DJ Baby mama

Lakini mbali na kukutana na changamoto hizo, bado Dj baby mama anaipenda sana kazi hii.

”Mimi ni Muislamu, na navaa hivi kwa kujiheshimu, watu wanaongea kuhusu heshima, mara napiga muziki nimevaa mabaibui, lakini haina shida maana ni kazi kama nyingine, kuna wengine wanafanya kazi za kawaida lakini kipato chao sio halali” anasema Aisha.

Alianza vipi kazi hii?

Aisha anasema kuwa anapenda sana muziki, na ameona kuna fursa hasa kwa wanawake wa visiwani vya Zanzibar, ndio akaamua kuanza shughuli hii ya kupiga muziki.

Kwanza alianza kama mtangazaji na mshereheshaji wa sherehe (MC), kisha akahamia katika shughuli ya kupiga muziki katika maeneo mbalimbali.

Amekua pia akiangalia katika mtandao namna ya kufanya shughuli za kupiga muziki ‘Dj’ kisha akaanza kufanya mazoezi.

”Napenda sana muziki, pia nimekua mtangazaji na mshereheshaji wa muziki, hivyo imekua rahisi kwangu kuingia katika kazi hii, hivyo huwa nasubiri sehemu kukiwa na kazi naambiwa kisha naenda kufanya”

Amepokea maoni gani kutokana na kazi hii?

Kwa upande wa familia yake, Aisha anaishi na mama yake, lakini hajui ni shughuli gani anaifanya, ingawa amekua akisikia kuwa binti yake anafanya kazi ya ‘Dj’ hajui hasa kazi hiyo ni ipi .

Aisha Bakari Mohamed
Aisha Bakari Mohamed maarufu kama DJ baby

”Mama yangu anasikia lakini hajui kama Dj huwa anafanya shughuli hizi, na mimi huwa namwambia naenda kwenye shughuli zangu za kusherehesha” anasema DJ huyo.

Baadhi ya watu wamekua wakimwambia kuwa hatakiwi kuchanganya mavazi ya hijabu na kupiga muziki, wakidai ni masuala ambayo hayaingiliani na ni kukosea heshima dini ya Kiislam.

”Ni jambo la ajabu, unavaa buibui halafu unapiga muziki kwenye vilabu, kwa binti wa Kiislam ni udhalilishaji” anasema Ally Juma mkazi wa Zanzibar.

Mbali na kupokea maoni hasi kwa kazi yake anayofanya, Aisha anasema kuwa hawezi kuacha kwani ni njia ya kujitafutia maisha na kusaidia familia yake.

”Niliwaza niache lakini siwezi kwasasa nimefika mbali sana na watu wengi wananijua, hapa ni kisiwa cha utalii kwa hivyo watu wa mataifa mbali mbali wananijua, siwezi kuacha fursa hii ipotee” anasema Aisha.

Chanzo BBC

By Ally Juma.Source link