Mmoja wa wafungwa walioachiwa kwa msamaha wa rais mkoani Njombe anashikiliwa na polisi mkoani hapa kwa kosa la kuvunja nyumba ya kulala wageni ya Nang’ano mjini Makambako ili kuiba fedha.

Mussa Msolwa maarufu Hitler amedai alikwenda hapo kulala lakini tamaa ilimshika baada ya kuona fedha hizo.

Jumatatu Desemba 9, 2019 Rais wa Tanzania John Magufuli alitoa msamaha kwa wafungwa 5,533 lakini mmoja wa wafungwa hao, Mussa Msola maarufu Hitler amekamatwa na polisi mkoani Njombe kwa tuhuma za kuvunja nyumba ya kulala wageni iliyopo mjini Makambako.

Msola ambaye kabla ya kuondoka katika gereza la Njombe aliomba msamaha mbele ya viongozi wa Serikali na maofisa usalama huku akiwasihi wenzake kuwa wema waendapo uraiani, aliachiwa huru jana Jumanne Desemba 10, 2019 saa 8 mchana.

Lakini saa nane baadaye alikamatwa na wananchi akiwa katika nyumba hiyo ya wageni ya Nang’ano iliyopo mtaa wa Mwembetogwa mjini Makambako akifanya uhalifu.

Rais Magufuli alitoa msamaha huo katika maadhimisho ya miaka 58 ya Uhuru wa Tanganyika yaliyofanyika uwanja wa CCM Kirumba mkoani Mwanza.

Akizungumzia tukio hilo leo Jumatano Desemba 11, 2019 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Hamisi Issa amesema, “ninaweza kusema msemo wa Kiswahili kuwa sikio la kufa halisikii dawa umetia leo Njombe baada ya mtuhumiwa mmoja Mussa Msola maarufu Hitler.”

“Aliyepewa msamaha (na Rais) na kuondoka Njombe kuja Makambako jana mchana lakini baada ya saa nane tangu atoke gerezani alishawishika na kufanya tukio la uvunjaji na wa nyumba ya kulala wageni ya Nang’ano.”

Issa amesema mtuhumiwa huyo ambaye kabla ya kutoa gerezani aliwasihi wenzake kuwa wema na kuomba msamaha kwa viongozi waliofika gerezani kushuhudia wafungwa wakiachiwa, alikamatwa na wananchi na kufikishwa kituo cha polisi.

“Yupo polisi na tulipomhoji alisema tamaa zimemshika na akafanya hayo. Tunawataka wasirudie vitendo vya uhalifu watarudi jela. Maisha yake ameamua kuwa gerezani na atarudi gerezani,” amesema Issa.Source link