Mwanaume anayeaminiwa kuwa ni Mkenya na ambaye anakisiwa kuwa na umri wa miaka 30 na zaidi aliyeanguka kutoka kwenye ndege ya Kenya Airways mjini LondonHaki miliki ya picha
MET POLICE

Image caption

Mwanaume anayeaminiwa kuwa ni Mkenya na ambaye anakisiwa kuwa na umri wa miaka 30 na zaidi aliyeanguka kutoka kwenye ndege ya Kenya Airways mjini London

Mamlaka ya Usimamizi wa Viwanja vya Ndege Kenya imepuuzilia mbali habari zilizochapishwa na shirika la utangazaji la Sky News la Uingereza kwamba mwanamume aliyeanguka kutoka ndege ya Kenya Airways ni Mkenya kwa jina Paul Manyasi.

Shirika hilo la habari lilisema uchunguzi wao umebaini mwanamume huyo huenda ni Paul Manyasi kutoka Kakamega, magharibi mwa Kenya.

Sky News walisema mwanamume huyo alikuwa anafanya kazi na kampuni ya Colnet Kenya ambayo imepewa kazi ya kufanya usafi katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta, Nairobi.

Lakini Mamlaka ya Usimamizi wa Viwanja vya Ndege Kenya (KAA) imesema hakuna mtu kama huyo aliyewahi kufanya kazi JKIA.

Colnet wamesema pia kwamba hawana mtu kama huyo aliywahi kufanya kazi nao.

Unaweza pia kusoma:

Hatua yao kukanusha kuhusu uwepo wa Paul Manyasi imezua maswali chungu nzima kuhusu nani hasa aliyejificha kwenye ndege hiyo na kuanguka kabla ya ndege hiyo kutua Heathrow, London.

Baadhi ya maswali yaliyojitokeza ni pamoja na utambulisho halisi wa mwanamume anayezungumziwa baada ya anayedaiwa kuwa babake kudai mwanawe yuko hai.

Paul Manyasi ni nani?

Sky News wanasema walipata kidokezo cha kwanza kutoka kwa dereva wa teksi za Uber kwa jina Kamau aliyewajulisha kwamba yupo mfanyakazi wa kampuni ya kufanya usafi ya Colnet aliyetoweka kipindi hicho. Alisema baadhi ya wafanyakazi walizungumzia kutoweka kwa mfanyakazi huyo.

Baadaye walikutana na mwanamke mfanyakazi wa Colnet ambaye hakutaka kutambuliwa, ambaye aliwaambia kwamba mwenzake kwa jina Paul Manyasi alitoweka mwishoni mwa Juni.

Haki miliki ya picha
MET POLICE

Image caption

Mkoba huu ulipatikana kwenye gia ya kutua ya ndege ambako mwanaume alikuwa alipodondoka kutoka kwenye ndege

“Mara ya mwisho kumuona, tulikuwa kazini, ghafla akatoweka, hakuna ajuaye alikoenda,” mwanamke huyo aliwaambia waandishi hao.

Anasema mkubwa wao kazini aliwaambia asubuhi iliyofuata kwamba yupo mtu aliyekuwa ametoweka lakini hawakuwa wanajua ni nani hasa na kwamba hilo lilifaa kuwekwa siri.

Mwanamke huyo alikuwa na picha za Paul na alisema walikuwa na uhusiano wa miaka miwili na walikuwa na mpango wa kuoana wakati mmoja.

Paul alikuwa anaishi mtaa wa Mukuru kwa Njenga pamoja na rafiki yake kwa jina Patrick ambaye ndiye aliyemsaidia Paul kupata kazi Colnet. Wawili hao wanatokea jimbo moja Kakamega.

Patrick anasema Paul alikuwa na ndoto ya kuondoka Kenya lakini hakuwahi kufichua alitaka kwenda wapi na ni kazi gani angeenda kuifanya.

Unaweza pia kusoma:

Picha mfano iliyotolewa na polisi wa London iliashiria muonekano wa mwanamume huyo aliyeanguka kutoka kwenye ndege. Walisambaza pia picha za vitu alivyokuwa navyo, ambavyo ni chupa ya maji na nyingine ya soda, na mkoba wa rangi ya kaki.

Mwanamke huyo alipooneshwa picha ya mwanamume huyo alisema wanafanana ila tu kwamba Paul hakuwa mweusi sana.

Alieleza aliutambua mkoba uliopatikana na kwamba maandishi MCA kwenye mkoba huo yalikuwa na maana ya Member of County Assembly (Mwakilishi wa wadi au Diwani), jina la utani ambalo Paul alikuwa akijiita.

Sky Net wanasema waliwasiliana na KAA na Colnet kuhusu taarifa walizokuwa wamezipata kabla ya kuchapisha makala yao, lakini mashirika hayo mawili hayakuwajibu chochote.

Wanasema walifika nyumbani kwao Paul Manyasi na wakakutana na babake Isaac Manyasi na mamake Janet.

‘Kuzuiliwa gerezani’

Waliwaambia kwamba hawajawasiliana na mwana wao tangu mwanzoni mwa Julai, jambo ambalo wanasema lilikuwa si la kawaida kwani angewapigia simu angalau mara moja kwa mwezi.

Wazazi hao walisema picha iliyotolewa ilifanana na ya Paul lakini hakuwa mweusi sana.

Haki miliki ya picha
MET POLICE

Image caption

Vitu hivi vilipatikana katika mkoba huu

Aliutambua mkoba, suruali ya ndani na viatu kwenye picha iliyotolewa na polisi.

Lakini babake amezungumza na runinga ya KTN anayesema kwamba hakukubali kwamba huyo alikuwa mwanawe.

Anasema mara ya mwisho kuwasiliana na mwanawe ilikuwa mwaka 2017 na kwamba baadaye alipokea habari kwamba mwanawe alikuwa anazuiliwa gereza la viwandani Nairobi takriban wiki moja iliyopita.

“Kijana wangu, mimi ninaamini kijana wangu ako,” amesema.

Alisema pia kwamba mwanawe huitwa Cedrick Shivanji , lakini anapanga kwenda Nairobi Ijumaa wiki hii kumtafuta mwanawe.

Baadhi ya picha zilizotumiwa kwenye makala ya Sky News kuwa ni za Paul Manyasi zinapatikana Facebook kwenye ukurasa wa mtu anayejiita Cedrick Junior.

Baadhi ya picha zilipakiwa kwenye Facebook mwishoni mwa Julai ilhali kisa cha mwili kuanguka kutoka kwenye ndege London kilitokea 30 Juni.

Kuingia uwanja wa ndege

KAA wanasema kwamba yeyote anayepewa kibali cha kuingia uwanja wa ndege, awe mwajiriwa au mfanyakazi wa kampuni za kibinafsi zilizopewa kandarasi, huwa amechunguzwa kabla ya kupewa kibali.

Wamesema kati ya wote waliokuwa wamepewa vibali, hakuna hata mmoja ambaye hajulikani aliko.

Hatua hiyo imeibua maswali kuhusu ni jinsi gani mwanamume huyo aliingia uwanja wa ndege hadi kufika kwenye ndege na kujificha.

Ni suala ambalo linaibua maswali kuhusu kiwango cha usalama JKIA. Je, kuna uwezekano kwamba alitumia kadi ya mtu mwingine au akatumia jina tofauti na jina lake halisi?

KAA wamesema uchunguzi bado unaendelea na kwamba wanatilia mkazo sana suala la usalama katika viwanja vya ndege.

Ukweli utajulikanaje?

Kwa sasa, wengi watasubiri kuona iwapo Isaac Munyasi atampata mwanawe katika gereza la viwandani.

Hilo lisipotokea, hatua itakayomaliza utata kuhusu iwapo aliyepatikana London ni mwanawe ni uchunguzi wa vinasaba au DNA.Source link