Phenny AwitiHaki miliki ya picha
Phenny Awiti

Image caption

Phenny Awiti

Phenny Awiti ni muathiriwa wa ugonjwa wa ukimwi kutoka nchini Kenya. Ni hali ambayo aligundua mwaka wa 2008 akiwa katika kidato cha pili wakati wa shughli za kupimwa ugonjwa wa ukimwi shuleni kwao na shirika moja.

Kujitolea kupimwa damu ilifuatwa na zawadi ya soda na mkate ambao ulikuwa ukitolewa na shirika hilo kama njia ya kuwafanya wanafunzi wengi kujitolea.

Na hapo ndipo utamu wa soda na mkate ulipelekea Phenny kuonja shubiri ambayo hakuitegemea.

“Wakati huo kitu ambacho nilifikiria sana ni kupata kula mkate na soda ambavyo vilikuwa vikitolewa. Kwa hivyo hata wakati nilipokuwa nashauriwa Kabla ya kupimwa, akilini nilikuwa naona wananipotezea wakati wa kupata mkate na soda.”

Punde si punde matokeo yalikuwa yametoka na yakaonyesha kwamba Phenny alikuwa na virusi vya ukimwi lakini matokeo hayo hayakuwa na nafasi akilini mwa Phenny kwasababu wakati huo angeweza tu kufikiri mkate na soda ambao ulikuwa kama dhahabu kwa wanafunzi waliosomea shule ya bweni.

” Mawazo ya kwamba nina virusi vya ukimwi yalianza kunisonga siku chache baadae.

Yaliponizidi nikaamua kumuelezea rafiki yangu niliyemuamini lakini habari kuhusu hali yangu ukaenea sana hadi kila mtu shuleni akajua kwamba ninaugua.”

Haki miliki ya picha
Phenny Awiti

Image caption

Phenny Awiti

Hata hivyo kitinda mimba huyu Kwa familia ya watoto sita alistaajabu kutambua kwamba ndugu zake walifahamu hali yake,lakini wakaliweka siri kwa sababu ambayo walielezea kwamba walishindwa kumueleza.

“Nilihisi kwamba simuamini mtu yeyote tena Kwa sababu nilihisi na nikamchukia sana mamangu na kumlaumu Kwa hali hiyo. Kwa sababu kati ya watoto sita, ni mimi pekee ndiye nina virusi”

Mazingira aliyokuwa Phenny yalimfanya kuwa mfungwa wa unyanyapaa.

” Kuna wakati ambapo nilikuwa na jipu kubwa kwenye tumbo yangu ambalo lilinisababisha kushindwa kutembea na nilipomwambia mmoja wa perfects ambaye alikuwa kwenye zamu akaniambia kwamba hatakinkujua kwamba nina ukimwi au sina, lazima Nitatembea. Nilijikunyata na kutembea pole pole hadi darasani. ” Anaelezea phenny.

Mbali na kwamba alilazimika kuficha dawa za kumeza kuepuka aibu ya kuonekana akimeza dawa za kupunguza makali ya Ukimwi (ARV), walimu pia hawakumsaza.

” Kuna walimu ambao walikuja darasani na kuuliza Phenny Awiti ni nani, kisha wangeondoka… Kumaanisha kwamba walikuwa wamesikia uvumi na walitaka kujua ni nani”

Ni Maisha ambayo alilazimika kuyaishi Kwa zaidi ya miaka miwili hadi alipokamilisha masomo. Lakini ni miaka ambayo aliyaishi kwa utundu.

” Nilikuwa mwanafunzi mwerevu lakini kutokana na jinsi mazingira yangu yalikuwa na mateso kiakili na kimwili, nilibadilika na kuwa mtundu. Niliamini kwamba utundu ungefanya ugonjwa kunitoweka”

Kama wasemavyo lisilobudi hubidi, Phenny alianza kuikubali hali yake na baada ya kumaliza shule ya upili alijiunga na masomo ya ziada anadai kwamba yalimsaidia hata zaidi kujikubali.

Haki miliki ya picha
Phenny Awiti

Image caption

Phenny Awiti

Ugonjwa wa ukimwi husambazwa Kwa njia ya ngono na mtu ambaye ana ugonjwa huo, mama kwa mtoto anapomnyonyesha na Kwa kutumia vifaa ambavyo vimetumiwa na mgonjwa wa ukimwi.

Phenny hata hivyo aliweza kujipatia mchumba ambaye alimkubali na hali take hata ingawa yeye mwenyewe hakuwa muathiriwa wa ugonjwa huo. Kwa kimombo uhusiano kama huu unajulikana kama ‘discordant couples’ . Miaka chache baadae ndoa yao ilivunjika.

” Nilikutana naye kupitia Kwa rafiki yangu. Na akanieleza kwamba ananipenda licha ya hali yangu na tukafanikiwa kupata watoto wawili wasio na ugonjwa huo, Faraja na Ahadi.

Mama Faraja anasisitiza kwamba ni kuzingatia matibabu ambayo yaliwawezesha watoto wake kutoambukizwa ugonjwa.

Mwaka 2017 Phenny alijitokeza wazi kuhusu hali yake kwenye mtandao wa Facebook.

“Wakati mmoja niliamka na kuhisi kwamba nimeçhoka kushinda nikielezea mtu mmoja mmoja kuhusu hali yangu na nikachapisha ujumbe mfupi wa kusema kwamba ninaishi na virusi vya Ukimwi… Nilikuwa na marafiki chini ya 15 lakini kilichonishangaza ni jinsi ujumbe huo ulivyosambaa kwa baraka na kuibua hisia nyingi kuhusu ugonjwa huo. Hapo ndipo nilipopata ari ya kuwa mwanaharakati wa masuala ya Ukimwi “

Kwa kutumia kurasa zake alianza kuhamasisha watu kuhusu ugonjwa wa ukimwi.

Mwezi uliopita mama Ahadi aliolewa na mpenzi wake ambaye pia anaishi na virusi vya ukimwi.

Phenny ambaye aliwashangaza wengi baada ya kufichua kwenye mitandao yake ya kijamii kwamba

ni mjamzito na anatarajia kupata mtoto wa tatu, anadai kwamba

“Ninataka kuwaonesha waathiriwa wengine kwamba mtu anayeishi na virusi vya Ukimwi ana uwezo wa kubeba mimba na kuzaa mtoto mwenye afya”

Lakini he hili linawezekana?

Nelson ni mtaalamu wa ugonjwa wa ukimwi kutoka shirika la

“Awali Kabla hata ya dawa za kupunguza makali ya Ukimwi kubuniwa, kina mama waliokuwa wanaishi na ugonjwa huo waliweza kujifungua watoto wengine wakiwa wameambukizwa na wengine wakiwa hawajaambukizwa… Ina maana kwamba maambukizi hutegemea viwango vya virusi. Maambukizi hufanyika wakati viwango vya virusi viko juu.

Na wakati mtu anatumia dawa za kupunguza makali ya Ukimwi, (ARV) viwango vya virusi hupungua hivyo kumuwezesha mama kumnyonyesha mtoto bila kumuambukiza virusi vya Ukimwi.”

Yote tisa, kumi ni kwamba bado watu wengi wanaougua ugonjwa huo wananyanyapaliwa katika jamii.

“Watu wengi wanaamini kwamba njia pekee ya mtu kuambukizwa ugonjwa wa Ukimwi ni kupitia kwa tendo la ndoa hasa kiukahaba, lakini si kweli. Kama mimi niliambukizwa na marehemu mamangu Lakini bado kuna watu kwenye mitandao ambao bado huniambia kwamba ninadanganya ila niliupata kupitia Kwa ukahaba…” Anasisitiza PhennySource link