Na SAMMY WAWERU

SWALI ikiwa mja amejipanga au kujiandaa na kujua atakachofanya siku za usoni baada ya kustaafu aghalabu huwa si rahisi kwa baadhi ya watu.

Wafanyakazi katika sekta binafsi na hata sekta ya umma wamekuwa wakihimizwa kuweka akiba katika Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii na Mafao (NSSF) ambalo wengi nchini Kenya hulifahamu kiurahisi wanapotajiwa ‘Hazina ya Uzeeni’.

Maisha ya uzeeni yanategemea jitihada unazotia au ulizotia katika umri wa ujanani. Ni muhimu kuwekeza, ili maisha ya uzeeni yasikupige chenga.

Kiinuamgongo, malipo baada ya kustaafu yanatolewa kwa minajili ya kuridhia utendakazi.

Pia, pensheni inalenga kujiendeleza kimaisha siku za usoni.

Uwekezaji unaweza ukawa kwa njia ya kuweka fedha katika mashirika ya kifedha kama vile benki au vyama vya ushirika, Sacco.

Njia nyinginezo ni kununua vipande vya ardhi, ploti na kujenga majumba ya watu katika familia zao au biashara huyatumia kwa kulipia kodi.

Kuna uwekezaji wengi hupuuza na ambao hauhitaji maelfu au mamilioni ya pesa kuupalilia; nao ni talanta.

Ni kipaji ambacho kinakolea akilini, mikono, macho, maskio na miguu ikiwa viungo vya kukifanikisha.

Mbali na kuwekeza kwenye mali, Mzee Samuel Chege amewekeza katika sanaa ya uundaji wa bidhaa. Ni talanta anayoendelea kuipalilia hata baada ya kustaafu.

Samuel Chege akiwa na mkewe na mwanagenzi, wakitengeneza bidhaa za kuvutia. Picha/ Sammy Waweru

Bw Chege amehudumu kama mpishi kwa zaidi ya miaka 25 katika taasisi mbalimbali. Ingawa alistaafu mwaka huu, kipaji chake katika uundaji wa bidhaa za urembo kwa shanga atakikulia maishani. Hutengeneza bidhaa kama vipochi, mikoba, mikufu na shanga pamoja na herini, kwa kutumia shanga za rangi tofauti.

Nguli huyu ambaye ni baba wa watoto sita pia huunda maboksi ya kuweka savieti na karatasi shashi nyinginezo, vichokoneo, sukari, chumvi na vijiko.

Kwa hakika hayo maboksi huwa yameundwa kwa njia ya kipekee.

“Pia hutengeneza vikapu vya sadaka na matoleo kanisani, mati za meza, trei za matunda na bidhaa za kula, na hutengeneza pia vifaa vya funguo; yaani vile vishikilio,” anasema.

Shughuli hizo anaziendeshea kiungani mwa jiji la Nairobi.

Katika mtaa wa Githurai, sebule yake ndiyo karakana ya gange hiyo.

Chege aliiingilia sanaa 2012 baada ya kutiwa motisha na mama mmoja aliyekuwa akitengeneza bidhaa za urembesho. “Nilivutiwa na sanaa tangu utotoni, hususan chini ya mtaala wa elimu wa zamani ambapo tulijifunza kufuma na kutengeneza vinyago,” asimulia.

“Mama huyo alinifunza vigezo kadhaa vya uundaji wa bidhaa za urembo. Zingine zimejiri kupitia ubunifu ninaouimarisha kila uchao,” Chege aeleza.

Anasema ilimgharimu mtaji wa Sh3,000 pekee, ambapo alianza kwa vikapu na pochi. Wakati huo aliifanya kama kazi ya ziada, kupiga jeki mapato yake. “Sanaa ni kazi ya akili, macho na mikono. Bidhaa zingine zilijiri baadaye nilivyoendelea kuimarika,” anasema.

Malighafi anayotumia ni shanga, kamba na glasi. Hutumia vifaa kama makasi na koleo kuendesha shughuli hiyo.

Mkewe Alice Wanjiru, pia amemfunza gange hiyo na amemfaa pakubwa katika kuifanikisha. “Ninafanya kazi za soko, wakati wa mapumziko hujishughulisha katika uundaji wa bidhaa,” Alice akasema wakati wa mahojiano.

Wawili hao hulenga hafla kama vile harusi na makanisa kuvumisha bidhaa zao.

Isitoshe, wana hupokea wanagenzi wenye ari ya kutaka kujua sanaa hiyo. “Nina watu kadhaa, wakiwamo watoto ninaowafunza kazi hii,” anasema Bw Chege.

Bidhaa zake hugharimu kati ya Sh100 hadi Sh5, 000.

Mjasirimali huyu anahimiza vijana kutilia mkazo na kupalilia talanta zao. Anasema ni uwekezaji usio na kikwazo chochote kifedha, na kwamba hauna kustaafu.

“Ninajivunia kipaji changu kwa kuwa kitanifaa maishani,” anasisitiza.Source link