Wanafunzi shuleni

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kwa kushirikiana na Center for Reproductive Rights kimewasilisha malalamiko kwa Kamati ya Wataalamu ya Haki na Ustawi wa Mtoto Afrika ((ACERWC)) kupinga kufukuzwa na kutengwa kwa wasichana wajawazito kutoka shule za umma nchini Tanzania.

Hatua hiyo inajiri baada ya rais John Pombe Mgufuli wa Tanzania kutoa agizo la kukataza wanafunzi wanaopata ujauzito na kujifungua kutoruhusiwa kuendelea na masomo.

Kulingana na mkurugenzi mkuu wa kituo hicho Evelyne Opondo hatua hiyo inakiuka mkataba wa Afrika kuhusu haki na ustawi wa mtoto na mikataba mingine ya haki za kibinadamu ambayo taifa hilo limeridhia.

“Kuwataka wasichana kufanyiwa vipimo vya ujauzito kinyume na ridhaa yao, kuwafukuza watoto shuleni mara baada ya kupata ujauzito na kuwazuia kurudi shule mara baada ya kujifungua ni uvunjifu wa haki yao ya msingi ya elimu na haki ya usawa bila ubaguzi,” alisema Bi Evelyne Opondo.

Mnamo Juni 2017, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Dkt. John Magufuli aliamsha upinzani mkali kutoka kwa watetezi wa haki za binadamu ndani na nje ya Tanzania baada ya kusema kuwa wanafunzi wanaopata ujauzito na kujifungua hawataruhusiwa kuendelea na masomo.

Akizungumza na waandishi wa habari mkurugenzi wa Utetezi na maboresho katika kituo cha sheria na haki za binbadamu Fulgence Massawe alisema kuwa wasichana wanaopata ujauzito wana haki ya kupata elimu na wanapaswa kuungwa mkono ili kusalia shuleni.

Mnamo mwezi Juni mwaka huu katika maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika jamii iliangazia changamoto zinazowakabili watoto katika bara la Afrika.

”Leo, tunachukua hatua kuitaka serikali ya Tanzania kuwajibika kwa kukiuka haki za wasichana na kuongezeka kwa mimba za utotoni nchini Tanzania”, aliongezea.

Kwa mujibu wa Utafiti wa Idadi ya Watu na Afya (TDHS) wa mwaka 2015-2016, mwanamke mmoja kati ya wanawake wanne wenye umri wa miaka 15 hadi 19 tayari wana watoto (mama).

Kulingana na matokeo hayo Elimu ya uzazi haitolewi mashuleni na wanafunzi wanasema kwamba hawana taarifa za msingi juu ya namna ya kujikinga na ujauzito.

Haki miliki ya picha
IKULU, Tanzania

Utafiti huo aidha umeongezea kwamba hadi kufikia sasa wasichana wengi wanazidi kupata mimba kwa sababu ya kubakwa na kwamba hakuna mtaala wa kitaifa wa elimu ya uzazi Tanzania Bara.

  • Mashirika yaitaka Tanzania kutowabana watetezi wa haki

Mwaka 2012 Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, pamoja na Shirika la Taifa la Usaidizi wa Kisheria, walifungua kesi dhidi ya Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa niaba ya wasichana wa shule nchini Tanzania, wakidai kuwa kuwapima wasichana ujauzito kwa lazima ni ukiukaji wa masharti ya Katiba ya Tanzania, hasa, Ibara ya 13 ya Katiba inayotoa haki ya usawa bila ubaguzi.

Mnamo Agosti 2017, karibu miaka mitano baada ya waombaji kufungua kesi, Mahakama Kuu ilifutilia mbali madai yao.

Mnamo mwaka 2013, Center for Reproductive Rights kilitoa chapisho lilipewa jina “Forced Out: Mandatory Pregnancy Testing and the Expulsion of Pregnant Students in Tanzanian” (Upimaji Mimba wa Lazima na Kufukuzwa Shule kwa Wanafunzi Wajawazito Tanzania) likionesha kwamba viongozi wa shule nchini Tanzania wanalazimika kuwafukuza wasichana wenye ujauzito shuleni.

Chapisho hilo pia lilitanabaisha kuwa kila mwaka, wastani wa wanafunzi 8,000 wa kike huacha shule kutokana na ujauzito. Kulazimishwa kupima mimba ni ukiukwaji mkubwa wa haki za wasichana za faragha na uhuru.Source link