MagufuliHaki miliki ya picha
IKULU TANZANIA

Image caption

Raisi wa Tanzania Dkt John Magufuli

Wafungwa katika magereza mbalimbali nchini Tanzania walionufaika na msamaha wa rais wameanza kutoka gerezani leo.

Vyombo vya habari nchini Tanzania vimeripoti na kutoa picha za wafungwa kutoka mikoa mbalimbali ikiwa ni pamoja na Mwanza, Lindi, Katavi, Dodoma, Arusha na mikoa mingine wakitoka katika magereza.

Baadhi wamenukuliwa wakimshukuru Rais John Magufuli kwa kuwapatia msamaha huo na kuahidi kuwa raia wema watakaporudi uraiani.

Jana katika maadhimisho ya miaka 58 ya uhuru, Rais Magufuli alitoa msamaha kwa wafungwa 5,533 nchi nzima ikiwa pia sehemu ya kupunguza msongamano gerezani.

Idadi hiyo ni kubwa kuwahi kutokea nchini, huku ikikaribia asilimia 15 ya wafungwa wote nchini.

Rais Magufuli alisema nchi nzima kuna wafungwa 35,803. Kati yao 17,547 ni wale ambao wamehukumiwa kwa vifungo vya muda tofauti huku 18,256 wakiwa bado wanasubiria hukumu ya kesi zao.

Alisema wapo baadhi watashangaa kwa uamuzi wake wa kuwaachia wafungwa wengi kiasi hicho lakini alidai kuwa ‘aliguswa moyoni’ kufanya hivyo.

Haki miliki ya picha
Getty Images

Image caption

Miongoni mwa wale walionufaika ni pamoja na wafungwa waliobakiza mwaka mmoja gerezani

“Baadhi ya wafungwa hao wamefungwa kwa makosa madogomadogo. Ameiba kuku, amemtukana rafiki yake kidogo, wamejibizana vibaya na mpenzi wake ama mshikaji wake. Wengine kwa kukosa mawakili wa kuwatetea vizuri kwenye kesi zao. Lakini wengine kwa kushindwa kulipa faini. Na wapo wengine wamefungwa kwa kuonewa,” alisema Rais Magufuli.

Wakati huo huo, baadhi ya vyombo vya habari vimeripoti juu ya mfungwa Merad Abraham akiwa na majeraha usoni baada ya kujijeruhi mwenyewe akishinikiza kubaki Gerezani.

“Sina pa kwenda, bora nibaki gerezani, ikiwezekana nitolewe hapa nihamishiwe Gereza la Ukonga Dar es Salaam lakini si uraiani,” amenukuliwa Abraham akisema.

Wanaharakati wa haki za binaadamu wameuita msamaha wa Rais Magufuli kuwa ni utaratibu wa kawaida wa kisheria na kuomba rais afikirie juu ya kupanua wigo wa msamaha huo kujumuisha mahabusu ambao kesi zao zimedumu kwa muda mrefu pasipo kutolewa hukumu.

Unaweza pia kusoma

  • Tete Kafunja: ‘Nilihukumiwa kunyongwa bila kosa’
  • Ni nchi ngapi ambazo bado zinatekeleza hukumu ya kifo?

“Rais ana uwezo wa kuzungumza na mwendesha mashtaka mkuu wa serikali (DPP) na kumshauri awaachie mahabusu ambao kesi zao zimedumu kwa muda mrefu kwasababu kama vile kuchelewa kupatikana kwa ushahidi wa makosa yao,” alisema Onesmo Olengurumwa, mratibu wa taifa wa shirika la wanasheria na watetezi wa haki za binadamu.

Watakaonufaika na msamaha wa Rais Magufuli ni pamoja na wale wamekuwa wakitumikia kifungo kisichozidi mwaka mmoja na wale ambao wamekuwa wakitumikia vifungo vya muda mrefu lakini wamebakiza muda usiozidi mwaka mmoja kumaliza kifungo chao.Source link